Ronaldo aikaribia rekodi nyingine ya ufungaji

Alhamisi , 10th Jun , 2021

Mchezaji bora wa Dunia mara tano raia wa Ureno Cristiano Ronaldo amebakiza mabao matano kufikia rekodi ya Gwiji wa soka wa zamani wa timu ya taifa ya Iran Ali Dael ya ufungaji bora wa muda wote kwa upande wa timu za taifa.

Ronaldo

Dael ndio mchezaji anaeongoza kufunga mabao mengi kwa upande wa timu za taifa kwenye michezo rasmi akiwa amefunga jumla ya mabao 109 akiwa na timu ya taifa ya Iran katika michezo 149, ambapo aliichezea timu yake ya taifa kuanzia mwaka 1993 mpaka 2006.

Jana Usiku katika mchezo wa kirafiki kati ya timu ya taifa ya Ureno na Israel Cristiano Ronaldo alifunga bao moja kwenye ushindi wa mabao 4-0 ambao Ureno waliupata, bao hilo limemfanya CR7 kufikishe idadi ya mabao 104 katika michezo 175, hivyo yamesalia mabao matano kuifikia rekodi ya Dael.

Ronaldo bado ananafasi ya kuongeza idadi ya mabao, kwani yupo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ureno kilichopo kwenye michouano ya Euro na wao ndio mabingwa watetezi. Na wataanza kibarua cha kuutetea ubingwa Juni 15 dhidi Hungary, wamepangwa wapo kundi F sambamba na mataifa ya Ujerumani na Ufaransa.