Jumamosi , 14th Mar , 2015

Wakati mashabiki wa soka waliofika katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam wakianza kutoka nje wakifikiri matokeo ya mchezo wa ligi kuu baina ya wenyeji Simba na wakata miwa Mtibwa sukari yataishia kwa suluhu mambo yakawa tofauti dakika ya mwisho

Mshambuliaji tegemeo wa timu ya Simba Emmanuel Okwi akiwatoka mabeki wa Mtibwa

Mshambuliaji hatari kipenzi cha mashabiki wa Simba Mganda Emmanuel Okwi maarufu kama 'Emo sting' alidhihirisha yeye ni shujaa wa wekundu wa Msimbazi Simba mara baada ya kuifungia timu hiyo bao pekee katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ngumu ya Mtibwa Sugar toka mkoani Morogoro katika mchezo mgumu uliopigwa katika uwanja wa taifa jijini
Dar es Salaam

Okwi alifunga goli hilo kwa shuti la mbali mpira uliogonga nguzo ya pembeni juu ya goli na kujaa nyavuni likiwa ni moja ya magoli yake bora au magoli bora yaliyofungwa katika ligi hii msimu huu akifunga goli hilo baada ya dakika 90 zikiwa zimebakia dakika 2 kati ya dakika 5 za nyongeza na kufanya mpira umalizike kwa Simba kuibuka kidedea kwa ushindi huo muhimu wa bao 1-0.

Katika mchezo huo mkali timu zote zilicheza kwa kushambuliana kwa zamu huku Simba ikikosa nafasi nyingi mpaka ilipopata bao hilo pekee kupitia kwa mshambuliaji wao Emmanuel Okwi ambaye wikiendi iliyopita alifunga goli pekee lililoipa Simba ushindi wa bao 1-0 dhidi ya mtani wake Yanga

Kwa matokeo hayo Simba imefikisha alama 29 moja nyuma ya Azam FC iliyo na alama 30 katika nafasi ya pili na mchezo mmoja dhidi ya Ndanda FC utakaopigwa siku ya Jumatatu katika uwanja wa Chamazi huku ikiwa nyuma alama 2 dhidi ya vinara Yanga wenye alama 31.