Jumatano , 27th Jul , 2016

Kocha wa Timu ya Ndanda FC ya Mjini Mtwara Joseph Lazaro amesema, atahakikisha anatumia mechi za kirafiki kwa ajili ya kutafuta wachezaji watakaoweza kuziba nafasi za wachezaji walioondoka ndani ya klabu hiyo ili kuiweka timu katika nafasi nzuri zaid

Kikosi cha Ndanda FC

Lazaro amesema, katika kikosi hicho ni wachezaji wengi walioondoka lakini atahakikisha anapata mechi za kirafiki kwa kipindi cha wiki moja kilichobakia kwa ajili ya kuangalia mapungufu yaliyopo ndani ya kikosi hicho ili kuhakikisha wachezaji atakaowaongeza wanafanya vizuri katika nafasi hizo.

Kwa upande mwingine Lazaro amesema, wamemchukua aliyekuwa kiungo wa Klabu ya Yanga Salum Telela ili kuhakikisha kiwango chake kinarudi kama hapo awali na kuweza kuleta changamoto ya kiushindani katika ligi.

Naye nahodha wa timu hiyo Kigi Makasi amesema, anaamini ligi itakuwa ngumu lakini wanaamini kwa kushirikiana na wachezaji waliosajiliwa wataweza kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita ili kuweza kujiweka katika nafasi za juu katika ligi hiyo.