Akizungumza leo Aprili 23, 2026, Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akipokea Ripoti ya Matukio ya Oktoba 29, 2025, Rais Samia amesema:
“Wapo waliotumia matokeo ya Oktoba 29, 2025 kutusimanga na kutunyooshea vidole, hatukushangaa sana kwa sababu mitazamo ya wanadamu haifanani, na kulikuwa na upotoshaji mkubwa wa habari za tukio hilo uliofanywa na vyombo vya habari hususani vya nje ya nchi na vya kimataifa, kwa desturi ya waungwana linapotokea jambo la hasara na kuumiza mioyo matarajio ni kufarijiwa badala ya kuzodolewa.”
Aidha, Rais Samia ameongeza kuwa maumivu ya matukio hayo yanabaki kwa wananchi wa Tanzania ambao ndio waliofikwa na masahibu hayo moja kwa moja.
“Kwa vyovyote vile walioumizwa na tukio lile ni sisi Watanzania, ni sisi tuliopoteza watoto wetu, ni sisi tuliopoteza ndugu zetu, haiwezekani mtu mwingine asiye Mtanzania awe na uchungu zaidi kuliko sisi Watanzania haiwezekani.”
Tukio hilo la upokeaji wa ripoti limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, huku ripoti hiyo ikitarajiwa kutoa mwanga wa hatua zinazofuata kufuatia matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojiri baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.


