Jumatano , 6th Dec , 2017

Kamati ya Olimpiki duniani IOC imeifungia Urusi kutoshiriki michuano ijayo ya Olimpiki Pyeongchang 2018, sambamba na kumfungia Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo Vitaly Mutko kutojihusisha na michezo hiyo maisha yake yote.

Vitaly Mutko ni waziri wa zamani wa michezo nchini Urusi aliyehudumu kuanzia mwaka 2008 hadi 2006 alipopata nafasi ya kuwa Naibu Waziri Mkuu.

Mutko amekumbana na rungu hilo baada ya ripoti ya uchunguzi kumkuta na hatia ya kukwamisha zoezi la mamlaka ya kuzuia dawa za kutunisha misuli michezoni (WADA) la kuwachunguza wanamichezo wa Urusi kwenye Olimpiki ya 2014 Sochi.

Bodi ya Utendaji ya IOC pia imewapiga marufuku wanariadha wa Urusi kushiriki michezo ya Olimpiki ya 2018 huko Pyeongchang, Korea ya Kusini lakini imetoa nafasi kwa wanariadha hao kushiriki kama wanamichezo binafsi na sio timu ya taifa.

Mwingine aliyekutana na kifungo cha maisha kutojihusisha na michezo ya Olimpiki ni Yuri Nagornykh, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa michezo akimsaidia Mutko wakati makosa hayo ya kukwamisha uchunguzi yakifanyika.

Naye rais wa shirikisho la Olimpiki nchini Urusi (ROC) Alexander Zhukov ameondolewa  uanachama wa IOC, wakati bosi wa zamani wa kamati ya Olimpiki ya Sochi 2014 Dmitry Chernyshenko ameondolewa kwenye kamati ya maandalizi ya Olimpiki ya Beijing 2022.