Jumanne , 30th Jun , 2015

Klabu ya Yanga imesema mchezaji Geofrey Mwasuya ni mchezaji halali wa Klabu hiyo ambaye amesajiliwa kwa kufuata sheria na kanuni za usajili na sio mchezaji wa Kimondo FC.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga Jerry Muro amesema, Mwasuya walikuwa naye muda mrefu ambapo baadaye alienda kuichezea Kimondo kwa mkataba wa kuichezea ligi hiyo na itakapomalizika mkataba unakuwa umefikia kikomo.

Muro amesema, hata kama Kimondo wanasema mchezaji huyo amesaini mkataba zaidi ya mwaka mmoja sio kweli kwani Ligi Daraja la kwanza mkataba wake unakwisha pale ligi inapofikia mwisho.

Kwa upande mwingine Muro amesema, upande wa wachezaji Donald Ngoma kutoka Zimbabwe na Joseph Zutta Tetteh kutoka nchini Ghana wamefuzu vipimo vya Afya na wamesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea klabu hiyo.