Ijumaa , 23rd Nov , 2018

Uongozi wa klabu ya Mtibwa Sugar umekana tuhuma za kucheza chini ya kiwango kwa makusudi katika michezo yake ya ligi kuu Tanzania bara kila inapofika mzunguko wa pili, ambao ni kuanzia Januari hadi Juni.

Kikosi cha Mtibwa Sugar

Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi wa klabu hiyo, Jamal Bayser alipohojiwa na www.eatv.tv, ambapo amesema kuwa hali hiyo huwa inatokea katika mpira kutokana na ushindani wa ligi, tofauti na watu wanavyochukulia kwamba inafanya kusudi.

"Suala hili kwamba Mtibwa inafanya makusudi sio la kweli, huwa inatokea katika masuala ya kimchezo, siku zote unaposhiriki katika mshindano ni kwa nia ya kushinda. Mpira una gharama sana na faraja pekee tunayopata ni ya kufanya vizuri, kwahiyo hatuwezi tukashiriki katika ligi kwa nia ya kufanya vibaya," amesema.

Pia, Bayser amezungumzia maandalizi ya Mtibwa Sugar katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika, akisema kwamba wachezaji wake pamoja na makocha wapo vizuri na wameshaanza na maandalizi kuhakikisha kwamba wanafanya vizuri katika ligi kuu pamoja na michuano hiyo.

Mtibwa Sugar iko katika maandalizi ya mwisho kwaajili ya michuano ya kimataifa wiki ijayo, ambapo itapambana na klabu ya Northen Dynamo ya nchini Ushelisheli. Mchezo wa kwanza ukitarajiwa kupigwa jijini Dar es salaam katika uwanja wa Chamazi ambao Mtibwa Sugar itautumia kama uwanja wake wa nyumbani.