Ijumaa , 18th Nov , 2016

Michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka nchini linalofahamika kama FA CUP itakayoshirikisha timu 86 msimu huu, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi rasmi hapo kesho kwa uzinduzi rasmi utakaofanyika mkoani Tanga.

Moja kati ya mechi za Kombe la FA, msimu uliopita

Uzinduzi huo utafanyika kwa kuzikutanisha Bingwa wa Mkoa wa Tanga, Muheza United na Sifa Politan ya Temeke, Dar es Salaam mchezo utakaopigwa katika Uwanja wa Mkwakwani jijini humo.

Michuano hii mwaka huu itashirikisha timu zote 16 za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, timu zote 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), timu zote 24 za Daraja la Pili (SDL) na timu 22 za mabingwa wa mikoa ambapo mashindano hayo yatakuwa ni ya mtoano na yataendeshwa kwa mizunguko tisa.

Mzunguko wa kwanza utashirikisha timu zote 22 za Mabingwa wa Mikoa katika makundi manne ya timu sita na timu tano ambako timu mbili za juu zitaingia raundi ya pili.

Mzunguko wa Pili utashirikisha timu nane zilizofuzu za RCL katika mzunguko wa kwanza na kujumuisha timu 24 za Daraja la Pili (SDL) kufanya jumla ya timu zote kuwa 32 kwa hatua ya pili.

Mizunguko mingine itafuata ambapo timu za ligi kuu zinaingia katika mzunguko wa 5, na hadi hadi hatua ya Fainali kutakuwa na jumla ya mizunguko 9