Jumanne , 1st Mar , 2016

Mashindano ya taifa ya mchezo wa kuogelea yanatarajiwa kuanza Jumamosi ya Machi tano mwaka huu kwa kushirikisha vilabu kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Katibu mkuu wa Chama cha Kuogelea TSA Ramadhan Namkoveka amesema, mashindano hayo yatatumika kwa ajili ya kupata wachezaji watakaoshiriki mashindano ya kuwania kufuzu ushiriki wa mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika nchini Brazili mwaka huu pamoja na kupata washiriki watakaoweza kushiriki mashindano ya CANA kanda ya nne.

Namkoveka amesema, pia mashindano hayo yataweza kutoa washiriki watakaoweza kushiriki mashindano ya dunia yatakayofanyika nchini Canada Desemba mwaka huu.

Namkoveka amesema, pamoja na mashindano hayo leo kamati ya utendaji ya TSA inakutana kwa ajili ya kuangalia maandalizi ya mashindano pamoja na kuipitia katiba ambayo inatarajiwa kupitishwa siku ya Jumamosi.