Alhamisi , 30th Jun , 2016

Baada ya kusubiriwa kwa muda mrefu ujio wa mshambuliaji mrefu raia wa Sweden aliyekuwa akikipiga katika klabu ya PSG ya Ufaransa, hatimaye kesho klabu ya Manchester United inatarajia kumtangaza rasmi Zlatan Ibrahimovic kuwa mchezaji wake mpya.

Mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic anayetajwa kujiunga na United.

Zlatan,34, atatangazwa Ijumaa hii kuwa mchezaji wa Man United iliyo chini ya kocha Mreno Jose Mourinho.

Raia huyo wa Sweden amemaliza mkataba wake na PSG ya Ufaransa ambako alifanya vema baada ya maisha yake ya soka akiwa Ajax nchini Uholanzi baadaye nchini Italia akiwa na Juventus, Inter Milan na AC Milan, pia Barcelona ya Hispania.

Taarifa zinaeleza kwamba Man United na Zlatan kila kitu kipo katika hatua za mwisho na kinachosubiriwa ni mkataba wake kumalizika rasmi hii leo na kesho Ijumaa atasaini mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo inayotumia dimba la kisasa la Old Trafold.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa mchezaji huyo ambaye aliisaidia timu yake ya PSG kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Ufaransa msimu huu akiifungia mabao 38 alishindwa kusaini mapema United kutokana na mkataba wake na PSG kuwa uko hai [active] na pengine angefanya hivyo kungemkosesha malipo ya bonasi.

Ibrahimovic atakuwa ni mchezaji wa pili kusajiliwa na kocha mpya wa United Jose Mourinho baada ya awali kocha huyo kufanikiwa kumsainisha kwa pauni milioni 30 beki wa kati raia wa Ivory Coast Eric Bailly kutoka Villareal ya Hispania.

Mourinho anataka kukiimarisha kikosi chake kwa kuongeza wachezaji wawili zaidi na tayari amepeleka ofa ya pili kwa kiungo fundi wa ushambuliaji wa Borussia Dortmund raia wa Armenia Henrik Mkhitaryan akiwa kwenye kipaumbele kikubwa cha kocha huyo.

United tayari imetuma ofa inayokadiriwa kufikia kiasi cha paundi milioni 26 kwaajili ya kiungo huyo tegemeo la klabu hiyo ya Ujerumani mwenye miaka 27 na sasa wanasubiri jibu juu ya usajili wake ambao unaonekana kwa asilimia kubwa utakamilika mwishoni mwa juma hili au mwanzoni mwa juma lijalo.