Kaimu kocha mkuu wa timu ya Simba Mganda Jackson Mayanja.
Bao pekee la mshambuliaji Hamisi Friday Kiiza ‘Diego’ limeipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda, Kiiza aliifungia Simba SC bao hilo dakika ya 6 kipindi cha kwanza kwa kichwa akimalizia krosi nzuri ya beki mwenye kasi wa upande wa kushoto Mohamed Husein maarufu kama Tshabalala ambaye alikimbia na mpira kwa kasi alioupokea kwa mshambuliaji galacha aliyekatika kiwango bora kwa sasa Ibrahim Ajib kutoka upande wa kushoto.
Na kwaushindi huo sasa Simba SC inafikisha pointi 30 baada ya kucheza mechi 14, ikiendelea kukaa nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga SC pointi 32 kwa mechi 13 na vinara Azam FC wenye pointi 35 kwa mechi 13 pia huku wao Azam FC wakitaraji kucheza mchezo wao usiku huu dhidi ya African Sports ya Tanga uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es alaam, wakati mabingwa watetezi Yanga SC wao watakuwa wenyeji wa Ndanda uwanja wa Taifa kesho Jumapili.
Pamoja na kufungwa, Mtibwa Sugar walionesha upinzani kwa Simba SC na dakika ya 11, kiungo Shiza Kichuya alipoteza nafasi ya wazi baada ya shuti lake kuokolewa na kipa Vincent Angban, raia wa Ivory Coast.
Dakika ya 44, Ally Shomari naye alipiga shuti kali, lakini kipa wa Simba SC, Vincent Angban akaokoa.
Kizza naye alipoteza nafasi za kufunga dakika ya 15 na 33 baada ya kupiga nje.
Kipindi cha pili, timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamani, lakini matokeo hayakubadilika.
Matokeo ya mechi nyingine za Ligi Kuu leo; Prisons imeifunga Toto 1-0 Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Stand United imeifunga 1-0 Kagera Sugar Uwanja wa Kambarage Shinyanga, Mbeya City imeifunga 1-0 Mwadui FC Uwanja wa Sokoine, Mbeya,Coastal Union imelazimishwa sare ya 1-1 na Majimaji Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.