Alhamisi , 23rd Mei , 2019

Kocha Mkuu wa klabu ya Yanga, Mwinyi Zahera, amefafanua namna ambavyo amejipanga kufumua kikosi chake kuelekea maandalizi ya msimu ujao wa ligi.

Kikosi cha Yanga

Akizungumza jana, mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu kati ya Yanga na Mbeya City ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, Zahera amesema kuwa atahakikisha anaweka wazi wachezaji wapya ambao klabu itawasajili kabla ya kuondoka kuelekea katika majukumu ya timu ya taifa ya Congo DR.

"Mimi naondoka Mei 28 usiku, kwahiyo wachezaji wote tunaowasajili msimu huu tutawatangaza tarehe hiyo ambayo nitaondoka. Wachezaji nane tayari wameshakubali, sita ni wa Kimataifa na wawili ni wa hapa ndani", amesema Zahera.

"Kuhusu wachezaji ambao tutawaacha, hiyo itajulikana katika mchezo wa mwisho dhidi ya Azam FC, kwahiyo mechi hiyo ikishamalizika mniulize wachezaji gani nitawaacha", ameongeza.

Pia amemzungumzia taarifa za kiungo mshambuliaji wa klabu hiyo, Ibrahim Ajib kujiunga na klabu ya TP Mazembe, ambapo amesema kuwa mchezaji huyo ni mzuri na anatakiwa kujituma kwakuwa yeye hatokuwa mchezaji mkubwa kama alivyokuwa Yanga.