Jumatatu , 2nd Aug , 2021

Mshambuliaji wa Tottenham Harry Kane hajaripoti mazoezini kwenye maandalizi ya timu hiyo kueleka msimu ujao wa 2021-22 kama ilivyokuwa imepangwa, tukio hili linahusisha uvumi wa kuwa mchezaji huyo anataka kuondoka klabu hapo akihusishwa kujiunga na Manchester City.

Harry Kane

Kane alipaswa kuripoti leo baada ya kumaliza mapumziko, mshambuliaji huyo alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya England kilichoshiriki michuano ya Euro 2020 na walifanikiwa kufika hatua ya fainali na kufungwa na Italia kwa mikwaju ya penati.

Mapema mwaka huu Harry Kane aliujuza uongozi wa Tottenham kuwa anataka kuondoka klabu hapo na amekuwa akihusishwa zaidi kujiunga na Manchester City ambao wapo tayari kutoa dau la pauni milioni 100 ambayo ni zaidi ya bilioni 322 za kitanzania. Lakini mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy anasema bila dau la pauni milioni 160 mchezaji huyo hauzwi, na tayari Manchester City walishapeleka ofa ya Pauni milioni 100 ofa ambayo Spurs waliikataa.

Kane mwenye umri wa miaka 28 alimaliza akiwa kinara wa ufungaji kwenye Ligi Kuu England EPL msimu uliopita baada ya kufunga mabao 23 kwenye michezo 35.