Jumamosi , 14th Jun , 2014

Bondia Ibra Class alikwenda nchini Zambia kimya kimya baada ya kuwepo mizengwe kutoka kwa baadhi ya watu aliodai kuwa hawapendi maendeleo yake na kuipeperusha vema bendera ya taifa ugenini kwa kurejea na mkanda wa ubingwa wa kimataifa wa WPBF.

Bondia Ibra Class 'King class mawe' akiwa na mkanda wa ubingwa wa WPBF alioutwaa baada ya kumchapa Mzambia.

Bondia chipukizi wa ngumi za kulipwa nchini Ibra Class 'King Class Mawe' ametua nchini akitokea nchini Zambia ambako alikwenda kuvaana na bondia kutoka Zambia kuwania mkanda wa ubingwa wa WPBF na kufanikiwa kutwaa mkanda huo baada ya kumtwanga kwa "Technical Knock Out" ya raundi ya tisa mpinzani wake.

Ibra Class amesema pambano hilo lilikua gumu hasa kutokana na uzoefu wa mpinzani wake ambaye alikuwa na faida ya kucheza nyumbani lakini hilo halikumzuia yeye kumsimamisha mpinzani wake huyo ambaye alikuwa akishangiliwa muda wote wa mpambano huo wa raundi 12 ambao uliishia katika raundi ya 9

Aidha Class amewataka mapromota kujitokeza kumwandalia mapambano mengi zaidi ya kimataifa na pia akatoa wito kwa mabondia chipukizi kote nchini kujiandaa vema ili kuwa "fiti" kwa michezo mbalimbali.

Naye promota wa bondia huyo Jay Msangi amesema ameamua kufanya kazi na bondia Ibra Class kwakuwa bondia huyo anajitambua na ni moja ya mabondia wenye malengo na mtazamo wa kufika mbali na alichokuwa akikosa bondia huyo ni sapoti ya watanzania hasa waratibu wa mapambano ili kukuza kipaji chake.