Ijumaa , 23rd Oct , 2015

Mshambuliaji wa TP Mazembe ya nchini Congo Thomas Ulimwengu amesema wanaamini mechi mbili za fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya USM Algier zitawajenga vizuri kuelekea mchezo kati ya Tanzania na Algeria.

Ulimwengu amesema wanacheza na timu moja ambayo ni bora Afrika na mechi itakuwa ngumu sana lakini kocha anajua afanye nini kuandaa wachezaji kuelekea mchezo huo na cha msingi wanatakiwa kuongeza umakini kwa kila jambo ambalo linaelekezwa.

Ulimwengu amesema, wachezaji wengine wa Taifa Stars ambao wanacheza ligi ya nyumbani wapatiwe maandalizi mazuri ili nao wawe vizuri kabla ya mchezo huo.

USM Algier watakuwa wenyeji wa Mazembe Oktoba 30 au Novemba 1, mwaka huu katika fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kurudiana Novemba 8 mjini Lubumbashi.

Na baada ya hapo, Samatta na Ulimwengu watajiunga na kambi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia Novemba 14, Dar es Salaam na Novemba 17 Algiers.