Jumatano , 7th Feb , 2018

Kocha wa zamani wa Barcelona Luis Enrique ameripotiwa kukubaliana maslahi binafsi tayari kwa kuchukua nafasi ya Antonio Conte kama kocha wa Chelsea.

Ripoti kutoka nchini Hispania zinaleza kuwa Enrique, ambaye pia amewahi kuzifundisha timu za Roma na Celta Vigo muda wowote anaweza kutangazwa kuwa kocha mpya wa Chelsea baada ya Conte kuwa na mwenendo mbaya.

Chelsea inashika nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na alama 50 kwenye mechi 26 lakini katika mechi mbili zilizopita imepokea vichapo vikubwa ambavyo ni 3-0 dhidi ya Bournemouth na 4-1 kutoka kwa Watford.

Moja ya michezo ya kwanza ya Enrique endapo atakuwa bosi wa Chelsea inaweza kuwa dhidi ya Barcelona kwenye dimba la Stamford Bridge Februari 20 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa hatua ya 16 kabla ya kurejeana Machi 14.

Akiwa Barcelona, Enrique alifanikiwa kutwaa makombe mawili ya La Liga, matatu ya Copa del Rey ikiwemo makombe matatu (Trebble) katika msimu wake wa kwanza ndani ya Barcelona.