Watu wanne akiwemo mama mjamzito wamenusurika kifo baada ya bajaji waliyokuwa wakisafiria kusombwa na maji katika Kata ya Malolo mkoani Tabora ikiwa ni athari ya mvua zinazoendelea kunyesha katika mkoa huo.
Akizungumzia tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia leo Disemba 28, 2025, dereva wa bajaji amesema, wakati akipeleka abiria hao, barabara ilikuwa imejaa maji hivyo hakujua vizuri mahali pakupita hali iliyosababisha maji kuizidi nguvu bajaji na kuwaburuza mtaroni yeye na abiria wake watatu.
Kwa Mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi hilo Loshipay Laizer, jeshi hilo limewaokoa watu hao kisha kuwapeleka katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tabora (Kitete), huku bajaji pia ikiokolewa licha ya kuharibika.
Kufuatia matukio hayo, Kamanda Loshipay Lazier amewasisitiza wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya majanga hayo hususani kipindi hiki cha mvua ili kuepusha madhara zaidi.

