Jumatatu , 23rd Jan , 2017

Nahodha wa Azam FC John Bocco amepanga kuipa heshima maalum Cosmopolitan leo katika mchezo wa Kombe la Shirikisho kwa kutoshangilia bao atakalofunga kutokana na kutambua mchango wao wa kumtoa hadi kusajiliwa na Azam FC.

John Bocco - Nahodha wa Azam FC

Bocco atakuwa akirejea kucheza dhidi ya timu yake hiyo ya zamani ambayo ndiyo imemtoa hadi kupata nafasi ya kusajiliwa na Azam FC miaka tisa iliyopita wakati ikishiriki ligi ya madaraja ya chini na kuipandisha rasmi Ligi Kuu mwaka 2008.

“Ni jambo zuri sana kucheza dhidi ya timu yako ya zamani, najisikia furaha sana ni moja ya mchezo mzuri kwangu na nitacheza kwa nguvu ili niweze kuisaidia timu yangu iweze kupata matokeo mazuri, siwezi kushangilia nikifunga bao, ile ni timu yangu ambayo imenitoa,” alisema.

Akizungumzia mchezo huo Bocco amesema kuwa wao kama wachezaji wana morali kubwa kwa ajili ya kucheza mchezo huo, huku akidai kuwa wamejipanga kupambana uwanjani kuhakikisha wanashinda mtanange huo.

Klabu hiyo bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa na kibarua cha kuzifuata Simba na Yanga ambazo tayari zimetangulia hatua ya 16 bora katika mchezo wa raundi ya tano ya michuano ya Kombe la Shirikisho utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Mechi nyingine zinazopigwa leo ni Stand United ambayo itacheza na Polisi Mara kwenye Uwanja wa Karume Mara wakati Ndanda itacheza na Mlale JKT kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.