Alhamisi , 8th Jun , 2017

AFC Leopards wamefuzu kuingia fainali ya Sportpesa Super Cup baada ya kuwachakaza Mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara, Yanga SC kwa mikwaju ya penati 4-2 mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Mchezaji wa AFC Leopards akiwa anafanya mashambulizi upande wa Yanga

Katika dakika 90 za mchezo, hakuna timu yoyote iliyoweza kuona nyavu za mwenzake kutokana na kila mmoja akiwa anamsoma mwenzake ili aweze kumuadhibu kutokana na mapungufu yake lakini juhudi hizo zilishindwa kuzaa matunda na hatimaye kuangukia katika mikwaju ya penati.

Kwa matokeo hayo timu ya AFC Leopards ya Kenya ndiyo timu ya kwanza kujikatia tiketi ya kuingia fainali ya michuano ya Sportpesa Super Cup ambapo itakuwa inamsubiri mshindi wa mechi ya pili inayoendelea sasa ili aweze kuungana naye katika fainali zinazotarajiwa kupigwa siku ya Jumapili June 11 mwaka huu.

Waliotumbukiza nyavuni matuta ya AFC Leopards ni Bernard Mango, Allan Katerega, Duncan Otieno na Dennis Shika wakati za Yanga zilifungwa na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kiungo mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa.

Chirwa mchezaji wa Yanga akijaribu kufanya mashambulizi upande wa AFC Leopards

Kikosi cha AFC Leopards kilikuwa; Ian Othieno, Shikai Dennis, Abwao Marcus, Mawira Joshua, Abdalla Salim, Othieno Duncan, Bernard Mango, Kateregga Allan, Uburu Vincent, Ramadan Yakoub, Fiamenyo Gilbert wachezaji waakiba wakiwa ni Edwin M, Nyakha A, Andrew T, Samuel N, Whyvonne I, Kiongera p, Ingotsi M, Andika G.

Yanga ni Nadir Haroub, Munish, Juma Abdul, Mohamed Ally, Andrew Vicent (Chikupe), Pato George (Ngonyani),Juma (Mahadhi), Maka Edward (Mwakalukwa), Obrey Chola (Chirwa), Yusuphu Antony (Mhilu), Emmanuel (Martin), Mbaraka Jumanne (Mfungo), Bakari Athman (Jomba), Said Juma (Ali), Said Mussa (Bakari), Samuel Greyson (Benkere), Festo Simon (Greson), Emmanuel Simon (Kichiba) pamoja na Babu Ally (Seif).

Katika hatua nyingine mashindano hayo ya SportPesa Super Cup yamekadiriwa kuteka hisia za wapenda soka na burudani zaidi ya Milioni 7 kwa siku mbili za kwanza za mchezo huo unaorushwa mubashara kupitia kampuni ya ITV na EATV.