Wachezaji wa Simba wakijadili jambo na kocha wao Masoud Djuma wakati wa mazoezi.
Masoud ameyasema hayo kwenye uwanja wa Boko Veteran jijini Dar es Salaam, ambako timu hiyo imeweka Kambi kwaajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza Juni 28.
''Huu mwaka tumesema hakuna mchezaji anasajiliwa Simba kuja kukaa benchi, atakaa benchi tu kwasababu kocha amefanya mabadiliko ya kikosi lakini hakuna mchezaji atakaa tu na kula mshahara, hilo hatulitaki'', amesema.
Masoud ameongeza kuwa michuano ya Klabu bingwa Afrika Mashariki na kati maarufu kama Kagame ataitumia kupima kikosi chake ili ajue naani atafaa kwenye eneo gani na endapo anakosekana mchezaji fulani asiwe na taabu kwenye kujua nani ataziba nafasi yake.
Simba ipo Kundi C na timu za Singida United, APR ya Rwanda na Dakadaha ya Somalia. Simba itafungua dimba na timu ya Dakadaha Julai 30, Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa. Hapo jana Simba imekamilisha usajili wa mshambuliaji Meddie Kagere kutoka Gor Mahia ya Kenya.