Ijumaa , 21st Jun , 2019

Ni kawaida katika miji mikubwa yenye msongamano wa watu katika nchi nyingi barani Afrika kukumbwa na adha ya usafiri wa raia wake.

Usafiri wa daladala

Nchini Tanzania, hali hiyo inaweza kuonekana zaidi katika majiji makubwa kama Dar es Salaam, Mwanza na Arusha, ambapo shida ya usafiri upelekea watu kujazana kwenye usafiri wa daladala ambao ndio unawapa unafuu watu wengi.

Kero kubwa ambayo imetajwa kuwachosha wanawake wengi kwenye daladala ni tabia ya baadhi ya wanaume kukaa nyuma yao, maarufu kwa jina la 'Kubambia', hali inayowafanya kukosa amani katika usafiri. 

Kupitia mada iliyowekwa katika ukurasa wa Facebook wa EATV, wanawake wengi waliotoa maoni yao wameonesha kukerwa na tabia hiyo, huku wengine wakidai kuwa baadhi ya wanaume hufanya makusudi ili tu waweze kutimiza haja zao.

Licha ya kero hiyo kwa wanawake wengi ambao wametoa maoni yao, kero zingine zinazowakera wasafiri wengi ni pamoja na nguo za makondakta wa daladala pamoja na usafi wao kwa ujumla kuwa mdogo, ambapo wamedai kuwa makondakta wengi si wasafi ilihali wao wanakuwa karibu mno na abiria. Pia suala la baadhi ya abiria kuzungumza lugha chafu kwenye daladala bila kujali rika zilizomo ni kero kubwa kwa abiria wengi.