Jumanne , 13th Sep , 2022

Benki ya NBC siku ya leo imechangia pakiti 3,000 za taulo za kike katika kampeni ya Namthamini inayoendeshwa na East Africa TV na East Africa Radio, ambazo zitakwenda kuwasaidia wanafunzi wa kike wapatao 250 kwa mwaka mzima.

Kutoka kushoto mtangazaji wa East Africa TV, Najma Paul akifuatiwa na Irene Peter ambaye ni Meneja wa huduma za jamii wa NBC akikabidhi taulo za kike kwa Meneja Mahuasiano wa IPP, Nancy Mwanyika na mwisho ni Justine Kessy mtangazaji wa East Africa Radio.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Meneja Huduma za Jamii wa NBC, Irene Peter amesema wamewasaidia wanafunzi 250 kwa kuwa wanathamini afya za watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao.

Benki ya NBC ni moja kati ya washirika wanaoisaidia kampeni ya Namthamini kwa mwaka 2022 ili kuwawezesha wanafunzi wa kike kutokosa masomo yao pindi wanapokuwa katika kipindi cha  hedhi.

Kwa upande wake Brenda Killeo ambaye ni Meneja Mawasiliano wa benki ya NBC amesema kampeni ya Namthamini ni miongoni mwa kampeni zenye thamani hapa nchini kwa kuwa inainua elimu na kuwafanya wanafunzi wa kike walio mashuleni kuwa majasiri na kutimiza ndoto zao ndiyo maana wameiunga mkono.