Jumatano , 11th Jul , 2018

Muigizaji nguli wa vichekesho kutoka kundi la Mizengwe, Mkwere Original ameweka wazi kuwa vipindi vya vichekesho katika runinga vitaendelea kuwa chaguo la kwanza kwa watazamaji na wapenzi wa vichekesho mbali na vichekesho vya mitandaoni.

msanii Mkwere

Mkwere amebainisha hayo wakati akizungumza na www.eatv.tv baada ya kuhojiwa kuwa kama wanapata changamoto ya kukosa watazamaji kulinganishwa na watazamaji wa mitandaoni.

"Kuna vipindi vya vichekesho katika runinga hufatiliwa sana na havijakosa mashabiki tangu miaka hadi sasa, wakiwemo watoto, wakubwa na wazee. Mfano baada ya igizo ninaloigiza mimi kuoneshwa, siku inayofuata unakuta mtazamaji ananihadithia mchezo ulivyokuwa mwanzo mwisho pia ananiita majina kutokana na uhusika niliocheza siku hiyo. Kwa hali hiyo vipindi kama hivyo ni vigumu kuacha kutazamwa” amesema  Mkwere.

Aidha muigizaji huyo amebainisha kuwa changamoto kubwa kwa baadhi ya vikundi vya uchekeshaji katika runinga  kushindwa kupata watazamaji wengi ni ukosefu wa maudhui ya kuelimisha katika vichekesho vyao.

Kuna watu wanachekesha lakini mazingira na mantiki ya vichekesho vyao havina elimu ndani yake, ndiyo maana unakuta watazamaji wengine wanahamia kwenye simu mitandaoni”, amesisitiza Mkwere.