Alhamisi , 19th Jul , 2018

Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), imempiga onyo msanii wa filamu nchini, Irene Uwoya kwa kitendo chake cha kuchapisha picha za nusu utupu kwenye mitandao huku wakimsisitizia kuwa endapo atarudia kufanya hivyo adhabu kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

msanii wa filamu nchini, Irene Uwoya

Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Vareli Msoka wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 19, 2018 Jijini Dar es Salaam na kumtaka msanii huyo kujitokea mbele ya jamii kutumia kurasa za mitandoni kuomba msamaha kwa kitendo ambacho amekifanya cha utovu wa kinidhamu pamoja na kuwa balozi mzuri kwa wenzake katika kutumia mitandao.

Akizungumza kwa upande wake, Irene Uwoya amekiri kufanya kukosa hilo na kuomba radhi huku akiitaka kamati hiyo ya maudhui kutoa semina kwa wasanii ili kuwapa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mitandao.

"Naomba nichukue nafasi hii kuomba radhi kwa nilichokifanya kwa kuweka picha ya nusu utupu, nina ahidi sitorudia kufanya hivyo tena", amesema Uwoya.

Mnamo Juni 20, 2018, Msanii Irene Uwoya alichapisha picha kwenye mtandao wake wa kijamii ikiwa inamuonyesha maungo yake ya ndani huku yeye mwenyewe alikuwa akidai alikuwa ufukweni ndio maana alifanya hivyo.

Muda mchache baada ya kumaliza kikao hicho Irene Uwoya alitekeleza sharti alilopewa na TCRA ya kutumia mtandao wake kuwaomba msamaha wananchi.

"Wapenzi wangu, ndugu zangu, wakubwa zangu na wadogo zangu naomba radhi kwa picha niliyopost. Najua niliwakwaza mnisamehe sana sikujua ntawakwaza nisababu tu ya role model wangu beyonce, nimejifunza sasa nawapenda", ameandika Uwoya.

Tokea TCRA iweke sheria za mitandaoni imekuwa ikiwaonya na kuwarudisha wasanii wengi kwenye mstari ulionyooka kwa kuwafundisha njia bora ya kutumia mitandao hiyo bila ya kuipotosha jamii kwa kuweka vitu ambavyo havina maana au visivyokuwa kwenye tamaduni za kitanzania.