Alhamisi , 3rd Dec , 2015

Msanii Menina amesema wasanii wa kike siku hizi wamekuwa wakionyeshana upendo tofauti na siku za nyuma, ambapo wasanii hao walikuwa hawana ushirikiano.

Menina ameyasema hayo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, na kusema kuwa wasanii hao wamebadilika na kutambua thamani zao, ingawa ushindani upo kwenye sanaa.

“Nadhani sasa hivi mfumo mzima umebadilika, wasanii wanapendana, wanasapotiana,wanakubaliana, yaaani kama msanii wa kike anamkubali msanii mwenzie wa kike na wa kiume anamkubali wakiume mwenzie, kwa hiyo vitu kama hivyo vipo katika sanaa kuna ushindani, sasa hivi kila mtu anajitambua anajua thamani yake kwa shabiki wake, kila mtu anajua kipaji chake ndio kinamfanya apendwe ama muonekano wake”, alisema Menina.

Menina aliendelea kusema hali hiyo inajidhihirisha wazi pale msanii anapotoa kazi mpya, na wasanii wenzake kupost kwenye mitandao yao ya kijamii, wakionyesha kumuunga mkono.