Alhamisi , 25th Feb , 2016

Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Charles Kitwanga amesema wataendelea kuwahamisha vituo vya kazi watumishi wa idara mbalimbali zilizopo chini ya wizara yake nchini lengo likiwa ni kuvuna mtandao wa ubadhirifu na rushwa.

Waziri wa mambo ya Ndani Mhe. Charles Kitwanga

Akitoa ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni ya kuwahamisha watumishi wa idara ya uhamiaji nchini waziri Kitwanga amesema kazi ya kuwahamisha watumishi imeanza jana na itakuwa endelevu na itahusisha watumishi waliokaa kwenye vituo vya kazi kwa zaidi ya miaka mitatu.

Waziri Kitwanga amesema zoezi hilo litaondoa watumishi waliojiwekea himaya ambao wanakuwa tayari wazoefu wa eneo hilo na kuweza kujikinga na mitego ya rushwa lakini pia zoezi hilo linalenga utendaji mzuri wa kazi pia.

Aidha Mhe. Kitwanga ameongeza kuwa hata ukusanyaji wa maduhuli pia unashuka kutokana na watumishi wengi kufanya kazi kwa mazoea lakini pia zoezi hilo linaipa wizara nafasi ya kuwachunguza watumishi ambao walikiuka taratibu za kazi ambao hawakuonekana kuhusika moja kwa moja kwenye ubadhirifu.

Waziri huyo ameongeza kuwa mazoea hayo pia huwa yanafanya watu wanaovuka mipaka mara kwa mara wasilipe ushuru au kodi za serikali kwa mtitiriko unaotakiwa kutokana na kuzoeana na watumishi wa mipakani.

Waziri Kitangwa amesema zoezi la uhamishaji wa watumishi wa idara hiyo limehusisha watendaji wadogowadogo lakini wale wakubwa ambao wamebainika na harufu ya utendaji mbovu na rushwa wamechukua hatua za kuwasimamisha.