Ijumaa , 25th Nov , 2016

Watu wenye ulemavu nchini wamedai kutoridhishwa na hali ya ujumuishi wao katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo, ikiwemo masuala ya kiuchumi, siasa, elimu, afya na fursa mbalimbali ambazo zitapelekea wao kujikwamua.

Felician Mkude - Katibu Mkuu SHIVYAWATA

Akiongea na East Africa Radio katika mahojiano maalumu jijini Dar es salaam, katibu mkuu wa shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania Felician Mkude amesema, watu wenye ulemavu wana haki sawa kama raia wengine kushiriki katika ajira na uzalishaji, lakini kutokana na taasisi na mashirika ya umma na yale ya binafsi kutokuwa na miundombinu wezeshi kwao ni miongonbi mwa suala ambalo linawanyima haki ya kushiriki kwenye uzalishaji na kutoajiriwa licha ya kuwa na ujuzi.

Waziri Jenista Mhagama na Naibu Waziri Dkt. Abdallah Posi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia wenye ulemavu

Felician amesema, katika tafiti waliyofanya kwa mkoa wa Dar es Salaam pekee inaonesha kuwa katika waajiriwa wote wa viwanda na mashirika mbalimbali ni asilimia 0.7 ya watu wenye ulemavu ndiyo wameajiriwa, huku kila watoto 10 wenye ulemavu 6 pekee ndiyo hupelekwa shuleni, hivyo kupelekea kundi hilo kukosa haki nyingi za msingi.

Aidha, ameiomba serikali kuhakikisha inashugulikia haki za watu wenye ulemavu kwa mujibu wa haki za binadamu na kwamba hakuna jambo lolote ambalo linawagusa watu wenye ulemavu litakalofanikiwa bila wao kushirikishwa kikamilifu.