Jumapili , 20th Jun , 2021

Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa Mhe. Ummy Mwalimu amesimamisha ujenzi wa miradi mitatu katika Halmashauri ya Kinondoni ikiwemo mradi wa ujenzi wa stendi ya Mabasi Mwenge kwa ajili ya uchunguzi.

Moja kati ya mradi wa Ujenzi wa kituo cha mabasi Mwenge amnao pia umesimamishwa.

Mhe. Ummy amefikia uamuzi huo mara baada ya kutembelea na kukagua miradi hiyo leo Juni 20, 2021 jijini Dar es Salaam ambapo amesema hajaridhishwa na ujenzi wa miradi hiyo kwani tangu ilipoanza hadi sasa imefikia asilimia 46 ya utekelezaji wake, licha ya kuongezewa muda.

''Sijaridhishwa na hatua za ujenzi wa stendi ya mabasi Mwenge, zipo sarakasi kwenye huu mradi zipo sintofahamu kubwa ili niweze kujiridhisha nasimamaisha ujenzi na naunda timu ya kuchunguza miradi yote mitatu stendi ya Mwenge, uwanja wa mpira pamoja na jengo la utawala wa Manispaa ya Kinondoni nataka kujiridhisha,'' amesema Waziri Ummy.

Pia Mhe. Ummy amemuagiza Katibu Mkuu TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe kumletea timu huru siku ya jumanne, tarehe 22/06/2021 kwa ajili ya kuchunguza mikataba yote kuanzia mwanzo ili kujiridhisha.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amemsimamisha kazi Mhandisi wa Manispaa Bwa. Isack Mpaki kuanzia leo .