
Prof. Joyce Ndalichako
Ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi wa mwongozo uliotolewa na Wizara ya Afya kwa wamiliki wa shule na wanafunzi wa kidato cha sita ambao shule zao zitafunguliwa kuanzia Juni Mosi kwa ajili ya kujiandaa kumalizia mitihani ya mwisho.
Prof. Ndalichako amesema kuwa Wizara ya Afya imetoa mwongozo ambao wanafunzi na wamiliki wa shule wanatakiwa kuufuata ikiwemo kuandaa sehemu za kunaniwia mikono shuleni na kama vitakasa mikono vitakuwepo basi vikidhi vigezo vya wizara, huku akipiga marufuku wanafunzi kubeba spirit shuleni.
"Wizara ya Afya imepiga marufuku wanafunzi kubeba spirit shuleni kwa sababu inaweza hata kuwaka moto na kuunguza mabweni lakini pia spirit ni kilevi mtu anaweza kutumia. Kwahiyo ni marufuku wanafunzi kwenda na spirit shuleni", amesema Prof. Ndalichako.
"Pia wazazi wanashauriwa wawapatie wanafunzi barakoa za vitambaa, ambazo wanaweza kufua na kunyoosha wakazivaa tena. Pia wanafunzi wanapaswa kuzingatia umbali watakapokuwa shuleni", ameongeza.
Waziri Ndalichako pia amepiga marufuku wamiliki wa shule kuwaagiza wanafunzi kubeba malimao na tangawizi na badala yake amewashauri kuwapa wanafunzi vyakula vyenye virutubisho sahihi.