Waziri aeleza sababu deni la serikali kuongezeka

Alhamisi , 10th Jun , 2021

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema sababu iliyopelekea deni la serikali kuongezeka kutoka shilingi trilioni 55.5 mwaka 2020 hadi kufikia shilingi trilioni 60.9 mwaka 2021, ni kutokana na kupokelewa kwa fedha za mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba,

Hayo ameyabianisha leo Juni 10, 2021, Bungeni Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020 na mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2021 hadi 2022, ambapo amesema licha ya deni kuongezeka lakini bado ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi wa kati na mrefu.

"Hadi Aprili 2021, deni la serikali lilikuwa shilingi trilioni 60.9, ikilinganishwa na shilingi trilioni 55.5 kipindi kama hicho mwaka 2020, kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi trilioni 43.7 na deni la ndani ni shilingi trilioni 17.3, ongezeko hilo lilitokana na kupokelewa kwa fedha za mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo," ameeleza Dkt. Nchemba.