Ghala la Samaki lililotembelewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Dkt. Kamani amesema lengo la soko hilo ni kuweka mazingira mazuri ya biashara ya samaki pamoja na kuwezesha serikali kukusanya ushuru wa bidhaa hiyo kirahisi.
Waziri wa mifugo na uvuvi, Dkt. Titus Kamani ametembelea mpaka wa Tunduma kujionea hali ya biashara ya samaki na mazao ya uvuvi kwenye mpaka huo, ambako ameshuhudia biashara hiyo ikifanyika kiholela, huku akielezwa na wenyeji wake kuwa suala la udhibiti wa biashara hiyo ni gumu kutokana na mazingira ya mpaka huo
Baada ya kujionea hali ya biashara ya samaki ilivyo katika mpaka huo wa Tunduma, Dkt. Kamani akatoa agizo la kuanza mchakato wa ujenzi wa soko la samaki mjini Tunduma ili kuweka mazingira mazuri ya biashara ya samaki na mazao ya uvuvi kwenye mpaka huo.
Mkurugenzi wa halmashauri ya mamlaka ya mji wa Tunduma, Juma Kitabuge, amesema kuwa tayari eneo la ujenzi wa soko la kisasa la samaki limeshapatikana na halmashauri inatafuta fedha za kuanza ujenzi huo.