Wazee wasiojiweza wanaohifadhiwa na serikali katika kambi maalum iliyopo eneo la Mwanzange jijini Tanga wameiomba serikali kuingilia kati tatizo la makundi hayo kunyimwa huduma za tiba katika hospitali za serikali hatua ambayo imechangia ongezeko la wazee hao kupoteza maisha.
Wakizungumza na katika kituo hicho kinachotegemea ruzuku kutoka serikalini kwa kushirikiana na wasamaria wema, wazee hao wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea wamesema mbali na ukosefu wa huduma za tiba pia kukosekana kwa usafiri wa kubeba wagonjwa katika kambi yao imekuwa ni changamoto kubwa kwao hasa wanapozidiwa nyakati za usiku.
Kwa upande wake msimamizi wa makao ya wazee wasiojiweza yanayosimamiwa na idara ya ustawi wa jamii
Bi. Otilia Chilumba amekiri kuwepo kwa changamoto hizo kwa wazee hao ambao baadhi yao wametokea jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Burundi na Rwanda hivyo amewaomba wasamaria wema kwa kushirikiana na serikali kusaidia changamoto hizo pamoja na ujenzi wa uzio kufuatia kambi hiyo kuingiliwa na watu hasa nyakati za usiku.
Kufuatia hatua hiyo jamii imeshauriwa kujenga tabia ya kuwathamini wazee hasa katika sekta za afya kwa sababu kila binadamu kulingana na kadri atakavyojaliwa kuishi duniani atakuwa mzee kama ilivyo kwa makundi hayo.