Jumapili , 17th Aug , 2014

Baadhi ya wazee wa mkoa wa Dar es salaam wamewataka watanzania kutowazomea wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba hasa wale wanaotokana pande hasimu za Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA na wale wa Tanzania Kwanza.

Baadhi ya viongozi wa kundi la wajumbe kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA.

Wazee hao wamedai kuwa kilichowakuta wajumbe hao ni nguvu za shetani kiasi cha kutojua mapenzi na jukumu lao kwa taifa kiasi cha kufikia hatua ya kutofautiana wakati wa kutekeleza jukumu muhimu kwa nchi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, kiongozi wa wazee hao Kapteni Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Alhaji Mohammed Ligora, amesema badala yake watanzania waombe Mungu aziunganishe pande hizo ili zifikie muafaka na kuendelea na mchakato wa katiba mpya.

Kwa mujibu wa Kapteni Mstaafu Ligora, mpasuko unaoendelea katika mchakato wa katiba mpya unachochewa zaidi na wanahabari kwa kushabikia moja kati ya pande hasimu katika mchakato huo.