Alhamisi , 15th Oct , 2015

Wazee wanaoishi katika kijiji cha King`ori wilaya ya Arumeru mkoani Arusha wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma za afya pamoja huduma ya maji safi pamoja na upatikanaji hafifu wa mahitaji muhimu ya chakula, mavazi na malazi.

Mzee Joshua Mbise mmoja wa wazee wa Kijiji cha Kong'ori Wilayani Arumeru Mkoani Arusha

Mzee Joshua Mbise Mkazi wa King`ori amesema kuwa kutokana uwezo mdogo wa kiuchumi wanashindwa kupata matibabu katika vituo vya afya hivyo wameiomba serikali iwasaidie waweze kupatiwa matibabu bila kutozwa gharama kubwa ili kunusuru afya zao

Mbise akizungumza katika zoezi la kukabidhi fedha za kupunguza umasikini katika kaya masikini linalofanywa na Mfuko wa TASAF amesema kuwa mbali na kuwa wazee pia wanategemewa na familia zao ambazo huziudumia licha ya kuwa na uwezo mdogo wa kufanya kazi kutokana na umri wao,Amesema kuwa Yeye binafsi atatumia fedha hizo kuanzisha mradi wa kuku wa kufuga ilia pate fed ha za kujikimu.

Kwa upande wake katibu tawala wa mkoa wa Arusha Ado Mapunda amesema kuwa katika kijiji hicho kimetengwa kiasi cha shilingi milioni 7 ambapo kwa mkoa wa Arusha kwa ujumla wenye kaya 44,000 zimetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1 na milioni 700 kwa ajili ya kupunguza umasikini.

Umasikini ni tatizo sugu katika nchi zinazoendelea hususan katika nchi ya Tanzania ambayo inashika nafasi za juu katika chati ya nchi masikini duniani,juhudi za TASAF huenda zikazaa matunda na kupunguza umasikini uliokithiri hasa maeneo ya vijijini ambapo watu hushindwa kupata milo mitatu.