Baadhi ya watuhumiwa akipelekwa Mahakani mjini Arusha
Jeshi la polisi nchini limewakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 16 wa uhalifu 9 kati yao wakihusishwa na tukio la milipuko ya bomu katika baa ya Night park jijini Arusha na wengine wa wakijihusisha na vikundi vya uhalifu vya ndani na nje ya nchi .
Mkurugenzi wa makosa ya jinai nchini kamishna Isaya Mgulu amesema kwenye kundi hilo watuhumiwa sita wanakabiliwa na tuhuma za kukusanya na kusafirisha vijana nje ya nchi kwa lengo la kujifunza uhalifu na mmoja kwa tuhuma za kufanya udanganyifu wa kupata hati ya kusafiria.
Kamanda mgulu amesema watuhumiwa 9 wanaohusishwa na mlipuko wa bomu katika baa ya nightpark wanakabiliwa na makosa ya jinai yakiwemo ya kuua na kujeruhi na watuhumiwa sita pia wanakabiliwa na makosa ya jinai yakiwemo kushawishi na kuwasafirisha vijana kujiunga na vikundi vya kigaidi ambapo tayari imeelezwa kwamba walishawasajili vijana 17 kwa ajili ya kujiunga na vikundi hivyo.
Baada ya taarifa ya DCI watuhumiwa hao walipandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mkoani Arusha na kusomewa mashtaka 17 ambapo watuhumiwa nane kati ya 16 wamesomewa mashtaka ya mauaji, watuhumiwa saba wakisomewa mashtaka kupanga na kuhamasisha vijana kujiunga na vikundi vya ugaidi na mmoja akishtakiwa kwa kufanya udanganyifu wa kupata hati ya kusafiria.
Baada ya kusomewa mahstaka hayo na hakimu Mustafa Siani akisaidiana na mwendesha mashtaka wa serikali Maselina Mwamunyange watuhumiwa 15 wa kesi za jinai hawakutakiwa kujibu lolote, wakati mtuhumiwa mmoja wa kosa la udanganyifu wa hati alikana shitaka linalomkabili .
Watuhumiwa wote wamepelekwa rumande na kesi ya watuhumiwa wa kushawishi vijana kujiunga na vikundi vya ugaidi itatajwa tarehe Juni 11 mwaka huu wakati wanaokabiliwa na shitaka la mauaji inatarajiwa kutajwa tarehe 12 Juni 12 mwaka huu.