
Baadhi ya watuhumiwa wakisubiri kusomewa mashitaka
Baada ya maombi ya Jamhuri pamoja na hoja za upande wa utetezi, mahakama hiyo imetoa dhamana kwa watuhumiwa hao wakiwemo baadhi ya wasanii waliokuwa wakishikiliwa na Jeshi la Polisi tangu mwishoni mwa wiki iliyopita.
Dhamana hiyo imetolewa na mahakimu wawili tofauti mahakamani hapo, ambapo katika shauri la kwanza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeridhia ombi lililowasilishwa na upande wa Jamuhuri la kuwataka watuhumiwa 5 wa dawa za kulevya kuwa chini ya uangalizi wa jeshi la polisi kwa kipindi cha miaka 3 na kuwasilisha dhamana ya shilingi milioni 20 pamoja na mdhamini mmoja kila moja na kisha kuachiwa huru.
Hakimu Mkazi Cyprian Mkeha ametoa dhamana hiyo kwa wasanii watano akiwemo, Ahmed Hashim a.k.a Petit Man, Lulu Abbas Chelangwa a.k.a Lulu Diva na Said Masoud a.k.a Said Alteza na wengine wawili ambao kwa pamoja wataachiwa huru baada ya kutimiza masharti ya kuwa na mdhamini moja kwa dhamana ya kiasi cha shilingi milioni 20.
Katika dhamana ya pili iliyotolewa na Hakimu mwingine ambaye ni Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Saidi kwa watuhumiwa 8 ambao ni pamoja na Rommy Jones, Khalid Mohamed a.k.a TID, Babuu wa Kitaa, Nyandu Tozzy, mwanadada Tunda, Lulu Diva, Recho na Joan, mahakama imeridhia ombi la Jamhuri na kuwataka kutoa dhamana ya shilingi milioni 10, na kufika kituo cha polisi mara mbili kwa mwezi kwa muda wa mwaka mmoja.
Awali jeshi la polisi liliwasilisha ombi hilo Mahakamani hapo kutaka watuhumiwa hao kusomewa kiapo cha mahakama ili waweze kuwa chini ya uangalizi kubaini kama wameachana na tabia hizo za utumiaji wa madawa ya kulevya na kuwa raia wema.
Kabla ya maamuzi hayo wakili wa upande wa utetezi Albert Msando analidai kuwa taarifa hizo hazijakamilika kwani hazioneshi wanaojiusisha na dawa za kulevya na walikamatwa lini na wapi na hakuna ushahidi wa kujitosheleza wa madai hayo kiasi cha wao kupata dhamana ya kuangaliwa tabia zao bila polisi kutoa ufafanuzi wa kina wa kwanini wanahitaji kupata dhamana ya uangalizi wa nidhamu.