
Kulingana na taarifa iliyotolewa na familia ya Lungu imethibitisha kuwa makubaliano yamefikiwa na serikali ambayo sasa yameruhusu Rais Hakainde Hichilema kusimamia mazishi ya serikali Jumapili ijayo.
Mzozo huo ulizua taharuki miongoni mwa baadhi ya watu nchini Zambia huku watu wakibaki wakishangaa jinsi ya kumuomboleza kiongozi wao wa zamani.
Edgar Lungu, ambaye aliiongoza Zambia kuanzia 2015 hadi 2021, alifariki siku 10 zilizopita nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa ambao haukujulikana.
Baada ya mazungumzo ya siku nyingi, familia ya Lungu na serikali wamekubaliana kwamba Mwili wa rais huyo wa zamani utasafirishwa hadi mji mkuu wa Zambia, Lusaka, siku ya Jumatano kwa ndege ya binafsi ya kukodi na baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege, mwili huo utapokelewa na familia na kisha kutakuwa na heshima kamili ya kijeshi.
Mwili Lungu unatarajiwa kupelekwa kwenye kituo cha mikutano katika mji mkuu ambapo umma utatoa heshima zao.
Mazishi ya kitaifa yatafanyika Jumapili Juni 22 na maombolezo rasmi yatakamilika siku inayofuata.
#EastAfricaTV