Jumamosi , 7th Oct , 2023

Watu tisa akiwemo mtendaji wa kijiji cha Kipengere, halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa makosa ya mauaji ya ndugu wawili mwaka 2020 kijiji hapo.

 

Hukumu hiyo imetolewa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe kwenye kesi ya mauaji namba 11 ya mwaka 2019 imetolewa na Hakimu Zabibu Mpangule mbele ya Washtakiwa, Mawakili wa utetezi na Mwendesha mashtaka ambapo amesema kwa kuzingatia makosa ya mauaji ya Watu wawili Francis Chaula na Fabio Chaula ambao ni Mtu na kaka yake Mahakama hiyo imewahukumu Washtakiwa wote kunyongwa hadi kufa.



Mahakama imesema mnamo April 27 , 2020 katika Kijiji cha Kipengere Washatkiwa wote waliwaua Francis Frank Chaula na Fabio Frank Chaula ambapo taarifa za uchunguzi wa miili hiyo iliyotolewa na Daktari ni kuwa sababu vifo vimetokana na kuvuja damu nyingi uliosababishwa kupigwa na vitu vizito.



Hakimu amesema mshtakiwa namba 6,7,8 na 9 ambao walikuwa ni Viongozi akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji, Mtendaji wa Kijiji pamoja na Mwenyekiti wa CCM wa Tawi wao wanaingia katika hukumu hiyo kutokana na kufanya vikao vilivyokuwa vikihusu mauaji kama ilivyoelezwa na mshtakiwa namba 5 kwenye kesi hiyo wakiwa na kisasi cha kumuua Frank Chaula kwasababu amekuwa akiwasumbua katika maeneo tofautitofauti.