Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefanikiwa kubaini majina ya jumla ya watu 52,000 waliojiandikisha zaidi ya mara moja kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kupitia mfumo wa Kielektroniki (BVR).
Taarifa hizo zimetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu wa tume hiyo na Mkuu wa Kitengo cha Tehama Dk. Sisti Karia wakati akitoa ufafanuzi juu ya zoezi la daftari la kudumu la wapigakura tangu uandikishaji, utoaji vitambulisho, uhakiki pamoja na utoaji wa orodha ya wapiga kura.
Dk. Karia amesema kuwa wamekabidhi kwa jeshi la polisi majina ya watu wote 52,000 waliofanya kosa la kujiandikisha zaidi ya mara moja kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Dk. Karia amefafanua kuwa watu hao wanakabiliwa na adhabu ya kifungo cha jela kisichopungua mwaka mmoja na nusu, pamoja na faini, na kuongeza kuwa tayari watu wengine 12 walishafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwenda jela.