Akizungumza katika mahojiano na East Africa Radio, Kibamba amesema hali hiyo imetokana na mapungufu yaliyomo kwenye sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010, inayoweka ukomo wa kiasi halisi cha gharama ambacho mgombea anastahili kutumia na ambayo amedai imekosa makali ya kuwashughulikia wanaokwenda kinyume na sheria hiyo.
Kwa mujibu wa Kibamba, baadhi ya wagombea wameshatumia zaidi ya fedha za Tanzania shilingi bilioni moja licha ya kuwa mchakato wa uchaguzi ndio kwanza unaanza na kwamba kuna kila dalili kwamba wanaweza kuvuka kiwango kikomo kilichowekwa na tume ya taifa ya uchaguzi.
Kibamba amesema ni mategemeo ya wengi kuwa sheria hiyo ingeanza kufanya kazi katika hatua za awali za mchakato wa uchaguzi ndani ya vyama, ambapo pia amezungumzia umuhimu wa wagombea kupimwa afya zao ili kuepuka gharama ambazo nchi inaweza kuziingia ikiwa ni pamoja na kulazimika kuahirishwa kwa uchaguzi iwapo mmoja ya wagombea atapata matatizo makubwa ya kiafya wakati wa kampeni.
Akifafanua kuhusu suala la afya, Kibamba amesema kuna haja Watanzania wakamteua kiongozi ambaye afya yake ni thabiti na itakayomwezesha kumudu madaraka ya urais na kwamba kuna uwezekano wa nchi kuingia gharama kubwa iwapo mmoja wa wagombea atafariki akiwa madarakani au hata wakati wa kampeni.
Ikitokea hali hiyo Kibamba amesema italazimu aidha kuahirishwa kwa kampeni za uchaguzi mkuu na kwamba iwapo kiongozi huyo atafariki akiwa jukwaani basi itabidi nchi iingie gharama mpya kabisa za kuitisha uchaguzi mwingine.
Wakati huo huo zoezi la kuchukua fomu za kuwania urais kwa tiketi ya CCM, limeendelea mkoani Dodoma ambapo hii leo makada sita wa chama hicho wamechukua fomu kutafuta ridhaa kupeperusha bendera ya chama hicho katika nafasi ya urais.
Makada wa CCM waliochukua fomu hii leo ni Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Mathias Chikawe na kufuatiwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Mhe. January Makamba na pia mbunge wa Sengerema Mhe. William Ngeleja.
Wengine waliochukua fomu za kuwania urais Bw. Boniface Ndengo, Mkulima kutoka Kigoma Edefonce Moshi Bilohe na wa mwisho hii leo kuchukua fomu ni Mkurugenzi Mstaafu wa Usalama wa Taifa Dk. Hassy Kitine ambaye alitangaza nia hii leo mapema akiwa Dodoma.