Mganga mkuu wa serikali ya Tanzania Mohamed Bakari ametoa wito kwa watanzania wote kuchukua tahadhari za kuthibiti na kujikinga na mazalia ya mbu hasa kwa kipindi hiki cha masika ili kujikinga na ugonjwa wa zika ugonjwa ambao unaenezwa na mbu.
Ametoa wito huo hii leo jijini Dar es salaama wakati akiongea na waandishi wa habari na kubainisha kuwa ugonjwa huo umekuwa tishio kubwa duniani kwani hauna kinga wala tiba huku vipimo vya kuubaini ugonjwa huo vikionekana ni ghari sana kwa nchi zinazoendelea.
Aidha shirika la afya la umoja wa mataifa limekusudia kufanya kikao wiki hii kujadili jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huo ili usienee sehemu nyingine za dunia kwani ugonjwa huu unahitaji jitihada za pamoja katika kukabiliana na ugonjwa huu.
Wakati huohuo kaimu katibu mkuu wa wizara ya afya Michael John amesema kuwa hali ya ugonjwa wa kipindupindu umepungua kwa asilimia 12 wiki hii huku mkoa wa Simiyu ukionekana kuwa na wagonjwa wengi zaidi, jumla kuu ya wagonjwa walioripotiwa wiki hii ni 459 na vifo 5 vimeripotiwa kutokea.



