Ijumaa , 25th Mar , 2016

Watanzania wameshauriwa kujenga utamaduni wa kununua nguo na mavazi mapya na kuacha tabia iliyojengeka ya kupenda kununua nguo zilizotumika maarufu kama mitumba.

Baadhi ya nguo mpya za watoto zikiwa zinauzwa dukani

Sambamba na hilo, wametakiwa pia kuacha wawazo potofu kwamba nguo mpya zinauzwa bei ghali ikilinganishwa na za mitumba na hivyo wakijikuta wakivaa nguo na viatu chakavu mara kwa mara.

Mfanyabiashara wa nguo kutoka eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam, Bw. Victor Mwansasu ametoa ushauri huo hii leo na kuonya kuwa nguo za mtumba ni hatari kwa afya kwani haijulikani aliyevaa kabla alikuwa ana matatizo gani ya kiafya ikiwemo magonjwa ya ngozi.

Kwa upande wake, mfanyabiashara Jackson Kulaba amelalamikia idadi ndogo ya wateja wanaokwenda kununua mavazi katika kipindi hiki kuelekea Sikukuu ya Pasaka huku akiihusisha hali hiyo na ugumu wa maisha.

Mfanyabiashara wa viatu Bw. Abuu Hassan Kaoye naye alikuwa na mawazo kama hayo lakini hakusita kuzungumzia tabia ya wazazi ambao hivi sasa wameacha utamaduni wa kufanya manunuzi kipindi cha sikukuu hususani viatu kwa watoto wao kama ilivyozoeleka miaka ya nyuma.