Jumamosi , 9th Apr , 2022

Baadhi ya wadau wa maendeleo nchini wameelezea faida na fursa za kuoneshwa kwa bunge mbashara hapa nchini.

Akizungumza na EATV mdau wa maendeleo, Peter Asenga amesema kuwa wananchi wanapaswa kufatilia vikao vya bunge hususani Bunge hili la bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ili kuelewa namna ambavyo miradi ya maendeleo itakavyotekelezwa na kufahamu zilipo fursa za kiuchumi na kijamii.

“Wananchi wanapaswa kutazama Bunge la bajeti linaloendelea kwa kuwa ni muhimu sana kwenye kutambua mabadiliko ya bajeti na kujua fursa zilizopo  kiuchumi na kijamii” Peter Asenga-Mdau wa Maendeleo.
Akigusia suala la ripoti ya uchunguzi ya mto Mara kupingwa vikali na wabunge amesema kuwa kitendo hicho kinatoa nafasi kwa wanasayansi kufanya utafiti wa kina na kuleta tija kwa taifa.

“Baada ya ripoti ya uchunguzi wa mto Mara kukataliwa Bungeni, hiyo imetoa tena fursa ya ajira  kwa wanasayansi kufanya utafiti wa kina kama kipo kilichojificha kwenye ripoti hiyo” Peter Asenga-Mdau wa Maendeleo.
Hata hivyo amewakumbusha baadhi ya wabunge wajibu wao wa kuwasemea wananchi shida zao na kuacha tabia ya  kukaa kimya bila kuchangia chochote kwenye vikao vya bunge.

“Kuna wabunge wamezoeleka kwa kuongea sana na wananchi wanapenda kuwasikiliza ili kujua atakuja na hoja gani, Inauma sana pale unapotegemea utamsikia Mbunge wa jimbo lako halafu husikii akichangia chochote, wabunge wanapaswa kuwakilisha shida za wananchi wao na sio kukaa kimya” Peter Asenga-Mdau wa Maendeleo.