Jumatatu , 16th Sep , 2024

Wazazi wamaoishi mtaa wa Saranga, kata ya Saranga jijini Dar es Salaam, wametakiwa kuwaonya watoto wao kuhusu tabia za wizi ambazo zimekuwa zikijirudia mara kwa mara na kupelekea wananchi kuwaza kuchukua sheria mkononi.

Wananchi wakichukua sheria mkononi

Wakiongea na EATV, wananchi wa Mtaa huo wanasema tabia za wizi zimekuwa kero kubwa kwani vijana wanaofanya vitendo hivyo wamekuwa wakitetewa na wazazi wao.
“Watoto wanaoiba tunaishi nao wazazi wao kila siku wanawatetea sasa ipo siku tutachoka maana tunawapeleka Polisi wazazi wao wanawatoa uvumilivu una mwisho siku tukija kuchoma mtoto wa mtu tusilaumiwe”, alisema Cassmir Marandu, Polisi Jamii Mtaa wa Saranga.

“Tunaomba Polisi watusaidie kwenye hili kwa maana huu wizi umekithiri sana mara Tv imeibiwa, mara simu zimeibiwa na wazazi wanakingia kifua watoto wao hata kama kweli hawana kazi lakini wizi sio kazi ambayo wananchi wanaweza kuivumilia”, alisema Rahim Zahoro, Mkazi wa Mtaa wa Saranga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo Godwin Muro anasema wamekuwa wakifanya mikutano kwa ajili ya kuwakumbusha wazazi kuwaonya watoto wao.
“Ni kweli kuna udokozi kwenye mitaa yetu na tunajitahidi kuimarisha ulinzi shirikishi lakini tunaliomba Jeshi la Polisi liwe linafika na huku labda udokozi huu utapungua”, alisema  Godwin Muro, Mwenyekiti Mtaa wa Saranga.

Aidha Muro anasema wananchi wakija kuchoka wasiilaumu Serikali.
“Niwaonye wazazi, uvumilivu una mipaka kuna siku hawa wanachi wanaoibiwa kila siku watachoka na vitendo hivi hawatowapeleka tena Polisi bali watachumua sheria mkononi na tumekuwa tukiwakataza kila siku kuchukua sheria mkononi lakini kuna siku watachoka na yanaweza kutokea madhara makubwa”, alisema  Godwin Muro, Mwenyekiti Mtaa wa Saranga.