Jumatano , 2nd Mar , 2016

Wananchi wa kata ya Tungi Manispaa ya Morogoro wamemuomba mwekezaji wa shamba la kampuni ya Tungi Estate kuwamegea sehemu ya shamba lake ili waweze kulima kufuatia kukosa eneo la kulima kwa zaidi ya miaka mitatu huku wakihofia baa la njaa.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt. Rajab Rutengwe

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara wananchi hao wamelalamikia serikali ya mkoa na wilaya kushindwa kuwasaidia kupata eneo kwa ajili ya kilimo huku wakituhumu uongozi wa mkoa kushirikiana na muwekezaji kuwafukuza katika mashamba yao ambapo wamemuomba waziri wa ardhi kuona uwezekano wa kuwatengea eneo maalumu.

Naye diwani wa kata hiyo bw. Juma Tembo, ameeleza hakuna haja ya wananchi hao kuendelea kuteseka kwa kutafuta eneo kwa ajili ya shughuli za kilimo hali ya kuwa manispaa hiyo ina mapori ya kutosha ya kuwatengea wakulima hao.

Akijibu malalamiko ya wakulima mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt. Rajab Rutengwe amesema hana mamlaka ya kumlazimisha mwekezaji kuwapa wakulima shamba bali watumie utaratibu wa kuandika barua ya kumuomba ndipo serikali ya mkoa itakuwa na nafasi ya kumshawishi muwekezaji huyo.