
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu Protabas Katambi akizungumza katika Siku ya VICOBA Tanzania iliyofanyika jijini Dar Es Salaam Septemba 23, 2023.
Katambi amesema katika kuboresha Uchumi wa Mtanzania Serikali imefanya masuala mbalimbali ikiwamo kuwa na Mpango Maalum wa kuwa na mifuko ya kukopesha wananchi ili kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha biashara na shughuli za kiuchumi mfano; Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Mfuko wa Pembejeo za kilimo
Naye Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamis amesema Wizara yake ina jukumu la kuratibu Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) unaotoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake. Mikopo hiyo imekuwa ikitolewa kwa riba ya 4% tu ili wanawake waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kuondoa utegemezi kwa wanaume.
Ameongeza kuwa Wizara inatekeleza Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo kwa lengo la kuimarisha shughuli za maendeleo ya jamii, masuala ya wanawake na jinsia, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, huduma za wazee pamoja na masuala ya ulinzi na usalama wa mtoto kwa lengo la kuwa na jamii yenye maendeleo endelevu.
Kwa upande wake Rais YEMCO VICOBA Tanzania Mohamed Basanga ameiomba Serikali kuweka uratibu katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri hasa kwa kuziangalia Taasisi ya Vicoba kuwezesha ziweze kuwalea wajasirimali wadogo wadogo katika kupata mikopo yenye riba nafuu ili kukuza bidhaa biashara zao.
"Mhe. mgeni rasmi nikuombe ufikishe salamu zetu kwa Rais Samia atukumbuke Taasisi za Vicoba katika fedha za Uwezeshaji ili ruweze kuwainua wajasirimali wengi na kujenga Uchumi wa Nchi" Amesema Basanga.