Jumapili , 30th Nov , 2014

Chama cha walimu Tanzania kimeitaka serikali kuwachukulia hatua zaidi wote waliohusika na wizi wa pesa za umma katika akaunti ya Escrow iliyokuwa Benki kuu kwa kulitia aibu taifa

Rais wa Chama cha Walimu Tanzania Gratian Mukoba

Chama cha Walimu nchini kimeitaka serikali kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na wizi wa fedha katika amana ya Escrow kwani kitendo hicho kimelifedhehesha na kulitia doa kubwa taifa na kuichafua serikali iliyo madarakani na pia kushusha morali wa kazi kwa watumishi waadilifu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mafinga Rais chama cha walimu nchini CWT. Mwl Gratian Mukoba amesema kitendo cha watu wachache wakiwemo viongozi wenye dhamana kujichotea fedha katika amana hiyo huku serikali ikiendelea kukimbizana na wananchi kutaka michango ya ujenzi wa maabara na kushindwa kuwashughulikia mafisadi hao, kinawakatisha tamaa watumishi waadilifu.

Aidha Mukoba ameitaka serikali kulipa fedha za makato ya mishahara ya walimu zilizotakiwa kulipwa kwenye SACCOS na wadeni mbalimbali zilizobakishwa hazina baada ya serikali kubadili utaratibu kwa kuwalipa watumishi mishahara moja kwa moja kwenye amana zao ambapo fedha hizo zililipwa bila makato hayo.

Akiwa katika ziara yake mkoani Iringa Rais huyo wa chama cha walimu nchini ameongoza harambee ya kuchangisha fedha kwaajili ya ujenzi wa ofisi ya chama hicho wilaya ya Mufindi na kufanikiwa kuchangisha zaidi ya shilingi milioni 17 huku yeye mwenyewe akichangia shilingi milioni Tano nukta moja

Tags: