Alhamisi , 28th Jan , 2016

Wakazi wa Mwakata wilayani Kahama Mkoani Shinyanga bado wanakubwa na kadhia ya kukosa makazi baada ya kukumbwa na mvua ya mawe iliyoua watu 42 na kujeruhi 91 mwaka jana 2015 mwezi Machi.

Hayo yamebainishwa Bungeni na Mbunge wa Msalala Ezekiel Maige (CCM) alipokuwa akichangia hotuba ya Rais Dkt. John Magufuli katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.

''Mheshimiwa Naibu Spika Baada ya maafa yale kutokea Rais aliyepita Jakaya Kikwete aliagiza wananchi wale wajengewe nyumba za kuishi ndani ya muda mfupi lakini hadi tunavyozungumza wananchi wale wanaishi kwenye maturubai jambo ambalo sii sahihi'' Amesema Maige

''Ahadi ya serikali ni ahadi ambayo inahitaji utekelezaji hivyo namuomba ndugu yangu Jenista Mhagama Bunge likimalizika twende pamoja jimboni ukajionee hali halisi ili serikali muanze kuwajengea nyumba wananchi hawa maana wanateseka na mvua zinazoendelea kunyesha''Ameongeza Maige.

Aidha Bunge linaendelea kuchangia hotuba ya Rais aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa Bunge Novemba mwaka jana ambapo wabunge wa upinzani wamesusia huku wabunge wa chama tawala wakiendelea kumpongeza Rais kwa hotuba nzuri kwa wananchi.