Ijumaa , 19th Dec , 2014

Wakazi wa Kiseke jijini Mwanza wanaoishi ndani ya eneo la mita 500 hadi kilometa moja toka eneo ulipojengwa mnara wa rada ya hali ya hewa, watakiwa kuhama ili kuepuka madhara ya kiafya yanayoweza kuwapata.

Kiseke jijini Mwanza

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania – TMA, kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Nguvu za Atomiki imewataka wakazi wa Kiseke jijini Mwanza wanaoishi ndani ya eneo la mita 500 hadi kilometa moja toka eneo ulipojengwa mnara wa rada ya hali ya hewa kuhama mara moja ili kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi pindi mtambo huo utakapoanza kazi rasmi.

Meneja wa mradi huo wa rada ya hali ya hewa, Mhandisi Lenny Mganga ameyasema hayo wakati akitoa maelezo kuhusu mradi huo ambao mpaka sasa umegharimu shilingi bilioni 3.6, kwa wajumbe wa bodi ya mamlaka ya hali ya hewa wanaokutana hapa jijini Mwanza katika kikao cha 39 cha bodi hiyo chini ya uenyekiti wa Morisson Mlaki.

Mhandisi Lenny Mganga ameongeza kuwa mradi wa rada hiyo pia unakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo za wananchi kuchimba kokoto na mchanga kuzunguka hifadhi ya mlima palipojengwa rada hiyo, shughuli ambazo amedai zinachangia uharibifu mkubwa wa mazingira na kuhatarisha uhai wa mradi, lakini pia akagusia changamoto ya kukatika mara kwa mara kwa umeme wa TANESCO.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Dkt. Agnes Kijazi amesema mazungumzo kati ya TANESCO na TMA, yanaendelea ili kuhakikisha pindi mtambo huo utakapoanza kufanya kazi kati ya mwezi Januari hadi Machi mwakani, pasiwe na tatizo lolote la kukatika kwa umeme ili mtambo huo uweze kufanya kazi vizuri.

Dkt. Kijazi pia amelezea sababu za mamlaka hiyo kujenga mradi mkubwa na wa kisasa wa rada katika mkoa wa Mwanza, huku mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya TMA Bw. Morisson Mlaki akifafanua suala la fidia kwa wananchi wa Kiseke waliojenga jirani na rada hiyo.