
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Shirika za Kimataifa la Atomiki la Utafiti wa Saratani (IARC) na Shirika la Afya Duniani ambazo zimetolewa leo mjini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ikiwa kesho ni siku ya Saratani Duniani na kusema kuwa kwa Tanzania tatizo la saratani limekuwa likiongezeka na kukua kila mwaka.
Amesema nchini Tanzania kila mwaka wagonjwa wapya wapatao 50,000 hugundulika na saratani za aina mbalimbali na kati ya hao ni wagonjwa 5,000 sawa na asilimia 10 ya wagonjwa wote ndiyo wanaofanikiwa kufika katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ili kuweza kupata tiba, huku asilimia 70 ya wagonjwa wanaobahatika kufika katika taasisi hiyo na kupata huduma za tiba hufika wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa.
Amesema tayari serikali imetoa shilingi bilioni tano kwa ajili ya ununuzi wa mashine mpya za mionzi ambazo zitasaidia kutibu wagonjwa wa saratani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage amesema sera ya Tanzania kwa ugonjwa wa saratani ni bure hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kupima ugonjwa huo kwani kama watawahi kupatiwa tiba inawezekana kupona kabisa tatizo hilo.
Kauli mbiu ya siku ya Saratani Duniani mwaka huu ni “Tunaweza, Ninaweza kwa Pamoja Tuwajibike Kupunguza Janga la Saratani Duniani”.
Msikilize hapa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Dodoma, leo